Ufugaji Bora wa Kuku wa Kienyeji - Part 1



Ufugaji wa kuku ni nyenzo nzuri ya kujipatia kipato katika kaya kwa sababu hauhitaji mtaji mkubwa na hauna kazi kubwa kiuendeshaji. Katika ufugaji huria kuku hujitafutia chakula wenyewe.

UTANGULIZI
Ufugaji wa kuku ni nyenzo nzuri ya kujipatia kipato katika kaya kwa sababu ufugaji wa kuku hauhitaji mtaji mkubwa na hauna kazi kubwa kiuendeshaji. Katika ufugaji huria kuku hujitafutia chakula wenyewe. Pia inapowezekana hupewa mabaki ya chakula, chenga, pumba au nafaka yoyote inayopatikana katika mazingira husika. Kwa walio wengi ifikapo nyakati za jioni, kuku hulala jikoni au ndani nyumbani kwa mfugaji mwenyewe. Ufugaji huu ni rahisi kwa kuwa hauna gharama kubwa ila faida yake ni kitoweo tu au fedha kidogo sana.

Tanzania ina idadi ya kuku wa kienyeji wanaokadiriwa kuwa million 34 ambao wanafugwa kwa mtindo wa huria. Ufugaji wa aina hii hufanyika vijijini na mijini pia. Idadi hii ya kuku bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Watanzania wanaokadiriwa kuwa milioni 40 (sensa ya mwaka ---). Ulaji wa nyama ya kuku nchini unakadiriwa kuwa ni wastani wa kilo 0.7 kwa kila mtu kwa mwaka mzima ilihali Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linakadiria wastani mzuri wa ulaji wa nyama kuwa ni kilo 6.8 kwa mtu kwa mwaka. Hii inaashiria kuwa soko la kuku nchini ni kubwa, ambayo ni fursa muhimu kwa wafugaji wa kuku.
ufugaji-wa-kuku-wa-kienyeji

Kutokana na lishe duni na kuzaana wenyewe kwa wenyewe (bila kubadili jogoo), kuku wa kienyeji walio wengi wana uzito mdogo. Wana wastani wa uzito wa robo tatu za kilo hadi kilo moja wakiwa na umri wa zaidi ya mwaka mmoja. Ila wakitunzwa vizuri zaidi na kuboreshwa wana uwezo wa kufikia uzito wa kilo moja hadi moja na nusu katika umri wa miezi sita hadi nane.
Kwa upande wa utagaji wa mayai kuku wa kienyeji kwa wastani hutaga mayai 50 hadi 65 kwa mwaka. Wakitunzwa vizuri zaidi huweza kufikia uzalishaji wa mayai 80 hadi 100 kwa mwaka.

NJIA ZA UFUGAJI WA KUKU

Mambo yanayomfanya mfugaji kuamua atumie njia fulani ya kufuga ni pamoja na uwezo wa kugharamia shughuli ya ufugaji wa kuku na ukubwa wa eneo alilonalo la kufugia. Katika sehemu hii utajifunza njia tatu za kufuga kuku ambazo ni:

1. Kufuga huria
Kuku huachwa wenyewe kujitafutia chakula na maji. Njia hii inatumika zaidi kufuga kuku wa kienyeji. Mara chache sana mfugaji huwapatia kuku chakula cha ziada. Kwa ufugaji huu lazima kuwe na eneo kubwa la kutosha kuku kuzunguka na kutafuta chakula. Kuku hulala eneo lisilo rasmi kama vile jikoni, kwenye kiambata n.k.

 Faida zake
• Ni njia rahisi ya kufuga.
• Gharama yake pia ni ndogo.
• Kuku wanapata mazoezi ya kutosha.
• Kuku wanapata chakula mchanganyiko ambacho kinafaa kiafya.

Hasara zake
• Kuku huwa hatarini kuibiwa au kudhurika na wanyama wakali na hali mbaya ya hewa.
• Ukuaji wa kuku ni hafifu, hufikia uzito wa kilo 1.2 baada ya mwaka.
• Huharibu mazingira kama kula na mimea ya bustanini mazao kama nafaka.
• Ni rahisi kuambukizwa magonjwa.

2. Kufuga nusu ndani – nusu nje
Huu ni mtindo wa kufuga ambapo kuku wanakuwa na banda lililounganishwa na uzio kwa upande wa mbele. Hapa kuku wanaweza kushinda ndani ya banda au nje ya banda wakiwa ndani ya uzio. Wakati wa mchana kuku huwa huru kushinda ndani ya banda hasa wanapotaka kutaga na wakati wa kuatamia au wanaweza kukaa ndani ya uzio nje.

Faida za kufuga nusu ndani na nusu nje
• Kuku wanakuwa salama mbali na maadui mbali mbali.
• Utaweza kuwalisha kuku wako vizuri hivyo wataweza kuongeza uzalishaji wa mayai na wa nyama (kwa kukua haraka).
• Itakuwa rahisi kwako kudhibiti wadudu na vimelea vinavyoweza kuleta magonjwa kwa kuku wako.
• Ni rahisi kuwatenganisha kuku katika makundi tofauti na kuwahudumia ipasavyo.
• Ni rahisi kutambua kuku wagonjwa kuliko kufuga huria.
• Kuku watapata mwanga wa jua wa kutosha pamoja na hewa safi.Wakati wa jua kali watakuwa huru kuingia ndani ya banda na kukaa kivulini.
• Kuku hawatafanya huharibifu wa mazao yako shambani au bustanini na kwa majirani zako.
• Utapata urahisi wa kukusanya na kupeleka mbolea bustanini au shambani.

Changamoto ya kufuga nusu ndani na nusu nje
• Huna budi uwe na muda wa kutosha kwa ajili ya kuwahudumia kuku wako.
• Pia utahitaji kuwa na eneo kubwa kiasi la kufugia.
• Pia utaingia gharama ya ziada kidogo ya kutengeneza banda na wigo na kuwapatia uku chakula cha ziada.
• Hata hivyo gharama za muda huo na za vifaa vingine zitafidiwa na mapato ya ziada utakayopata kwa kufuga kwa njia hii.

3. Kufuga ndani ya Banda tu
Njia nyingine ni kuwafuga kuku ndani tu. Katika njia hii, kuku hukaa ndani wakati wote. Njia hii ya ufugaji utumiwa zaidi na wafugaji wa kuku wa kisasa. Lakini yaweza kutumika hata kwa kuku wa asili hasa katika sehemu zenye ufinyu wa maeneo.

Changamoto za ufugaji wa ndani ya banda tu
• Unatakiwa uwe na muda wa kutosha wa kuwahudumia kuku wako kikamilifu.
• Pia unatakiwa kuwa na mtaji mkubwa wa kujenga banda na kuwanunulia kuku chakula.
• Ugonjwa ukiingia na rahisi kuambukizana.Vilevile kuku huweza kuanza tabia mbaya kama kudonoana, n.k.

Faida za kufuga ndani tu
• Ni rahisi kutambua na kudhibiti magonjwa.
• Ni rahisi kudhibiti upotevu wa kuku, mayai na vifaranga.
• Ni rahisi kuwapatia chakula kulingana na mahitaji ya kila kundi.
• Ni rahisi kuwatambua na kuwaondoa kuku wasiozalisha katika kundi.

Ni ufugaji upi unafaa zaidi kutumika kwenye mazingira ya vijijini?
Kwa ujumla, njia rahisi na inayopendekezwa kutumiwa na mfugaji wa kawaida kijijini ni ya ufugaji wa nusu ndani na nusu nje, yaani nusu huria. Hii inatokana na faida zake kama zilizoainishwa hapo awali. Kwa kutumia mfumo huu wa ufugaji, utaepuka hasara za kufuga kwa mtindo wa huria kama zilivyainishwa mwanzoni mwa makala hii. Pia ukitumia mtindo wa ufugaji wa nusu huria utafanya ufugaji wako kwa njia bora zaidi ndani ya uwezo ulionao, kwa sababu kwa sehemu kubwa utatumia mali ghafi inayopatikana katika eneo lako.

BANDA LA KUKU

Sifa za banda bora la Kuku
Ukiamua kufuga katika banda kwa njia mbili zilizoelezwa awali utatakiwa kujenga banda lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi ya kuku. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa
kama ifuatavyo:

i) Liwe jengo imara
• Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
• Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
• Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
• Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.

ii) Liwe rahisi kusafisha
• Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
• Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
• Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au Maranda ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako.
• Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
• Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.

iii) Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.

iv) Liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.

v) Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti magonjwa.

vi) Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa (kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku. Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.

vi) Paa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia mchoro hapa chini).

Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu view katika banda:


i) Vyombo vya Maji
Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.
• Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
• Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafi liwe kirahisi.
• Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.

ii) Vyombo vya Chakula
Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini. Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.

iii) Viota
Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao (angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.

Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja (angalia picha hapa chini). Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota. Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.

iv) Vichanja
Kuku wana asili ya kupenda kulala au kupumzika sehemu iliyoinuka. Hivyo ndani ya banda weka vichanja vitakavyotosheleza idadi ya kuku waliopo.


SOMA: Ufugaji wa kuku wa kienyeji - Part 2

Comments

Top Jobs that others viewed

JOB VACANCIES: AGRICULTURE

NAFASI YA KAZI: Meneja wa Shamba